Wabunge Esther Bulaya pamoja Halima Mdee ambao ni washtakiwa katika kesi ya jinai namba 112 ya mwaka 2018 ikiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko usio halali kinyume cha sheria wameshindwa kufika mahakamani leo kutokana na usafiri waliokuwa wakitumia kupata matatizo.
Hayo yamebainishwa na Wakili wa utetezi, Peter Kibatala mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, kuwa sababu ya washtakiwa hao kutokuwapo mahakamani imetokana na usafiri waliokuwa wanatumia kutoka bungeni mjini Dodoma kuelekea Dar es Salaam, kuwa na tatizo na kusababisha wachelewe kufika.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 112 ya mwaka 2018 inayowakabili viongozi tisa wa CHADEMA, akiwamo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe Halima Mdee , ni mshtakiwa wa saba, na Ester Bulaya ni mshtakiwa wa tisa.
Mbali na Bulaya pamoja na Mdee washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji , Mbunge wa Iringa Mjini Mch. Peter Msigwa, Naibu makatibu wakuu Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara), Mbunge wa Tarime Mjini Esther Matiko, na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.
Viongozi hao wa CHADEMA wanakabiliwa na mashtaka 12 katika hiyo ya kufanya mkusanyiko na maandamano yasiyo halali Februari 16, 2018 yaliyosababisha kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline.