Wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliosimamishwa kuhudhuria Bunge kwa mwaka mmoja, Ester Bulaya wa Bunda na Halima Mdee wa Kawe, wamemfikisha mahakamani Spika wa Bunge, Job Ndugai, wakipinga kusimamishwa kwao.
Mwingine ambaye wamemfikisha mahakamani ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge, George Mkuchika, ambaye ni Mbunge wa Newala Mjini (CCM).
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa tayari wabunge hao wamewasilisha shauri lao kwenye Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma.
John Mnyika ambaye alisimamishwa kuhudhuria vikao vya siku saba, adhabu ambayo ilishaisha, naye ameungana na wabunge hao kwenye kesi hiyo.
Lissu alisema waombaji wanaiomba mahakama kuu itoe amri ya kufuta uamuzi wa Spika na wa Bunge kuwasimamisha John Mnyika kwa vikao saba na vile vile ifute kabisa uamuzi wa Bunge wa kuwasimamisha kuhudhuria vikao vilivyobaki na vikao vyote vya Mkutano wa nane na vikao vyote vya Bunge la Tisa, Ester Bulaya na Halima Mdee.
Lissu alisema adhabu zote hizo zinakwenda kinyume na sheria na zilitolewa na Bunge hilo kama kuwakomoa wabunge hao watatu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Mdee na Bulaya wamefungiwa kuhudhuria vikao vyote vilivyobaki vya Bunge hili na watakuwa nje mpaka Aprili mwakani.