Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imeanza mchakato wa ujenzi wa vyumba vya upasuaji kwa ajili ya kutoa huduma ya upandikizaji wa figo nchini.
Taarifa hiyo imetolewa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangalla, wakati akifungua mkutano wa tatu wa Chama cha Wataalamu wa Figo Tanzania (NESOT), uliofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.
Dk Kigwangalla alisema kuwa wizara yake imekuwa ikilipia gharama kubwa za matibabu ya wagonjwa wa figo wanaohitaji huduma ya upandikizaji, kutokana na huduma hiyo kutolewa nje ya nchi.
Amesema kutokana na huduma hiyo kutopatikana nchini, hadi sasa zaidi ya wagonjwa 250 wamepatiwa huduma ya kupandikizwa figo ambapo wizara imekuwa ikigharamia matibabu hayo.
Dk Kigwangalla amesema Serikali ya Awamu ya Nne ilielekeza nguvu zake katika kujenga kituo cha magonjwa ya moyo na upasuaji, ambapo hapo awali Watanzania walikuwa wakipata huduma hiyo nje ya nchi kwa gharama kubwa zaidi.
Amesema kwa kutambua umuhimu wa huduma za figo nchini, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepeleka wataalamu wa afya nchini India kwa mafunzo ya muda mfupi, ambao ni madaktari wa figo, madaktari wa upasuaji, wauguzi na wataalamu wa maabara.