Mahakama ya wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro imemhukumu mbunge wa jimbo la Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali kwenda jela miezi sita bila faini baada ya kukutwa na hatia ya kuwafanyia fujo polisi wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Mbunge huyo na dereva wake, John Bikasa wamekutwa na hatia ya kukata utepe wa polisi na kuwafanyia fujo jambo ambalo ni kinyume na sheria.
Kama hatokata rufaa dhidi ya hukumu hiyo mbunge huyo atapoteza sifa za kuendelea kuwa mbunge, kwa sababu kisheria, mbunge hatakiwi kuwa na historia ya kukutwa na hatia ya kosa lolote la jinai.
Kabla ya tukio hilo, Mheshimiwa Lijualikali, amewahi kuingia matatizoni na polisi, baada ya Machi Mosi, 2016, kukamatwa na polisi na kuswekwa rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi, Wilaya ya Kilombero kwa madai ya kuingia katika uchaguzi wa Baraza la Madiwani wilayani humo wakati ikidaiwa kwamba hakuwa na sifa za kuingia.