Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali na viongozi watatu wa Chadema wilayani Malinyi wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufanya kusanyiko lisilo halali.
Mbunge huyo amekamatwa jana jioni wakati akitoka kwenye kikao cha ndani cha chama hicho kilichofanyika katika Kijiji cha Makerere wilayani Malinyi.
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, Alfonce Mbassa amesema baada ya kumaliza kikao, mbunge huyo na viongozi wengine walipanda kwenye magari ili kuondoka lakini ghafla lilitokea gari la polisi na askari walimuamuru Lijualikali ashuke.
Amesema walijaribu kuwaelewesha polisi kwamba kilikuwa ni kikao cha ndani lakini askari walisisitiza kuwa lilikuwa kusanyiko lisilo halali.
Amewataja waliokamatwa pamoja na mbunge huyo kuwa ni Mwenyekiti wa Chadema Malinyi, Emmanuel Lukindo; Katibu wake, Sadi Lyampawe na Katibu wa Uenezi wa wilaya, Lucas Lyambalimu.
Alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo, mkuu wa wilaya Kasika amesema ni kweli ameagiza polisi kumkamata mbunge huyo kwa kuwa anafanya siasa nje ya jimbo lake.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leons Rwegasira amesema hajapata taarifa za kukamatwa kwa mbunge huyo.