Mbunge wa Viti Maalum, Catherine Ruge (Chadema), aliyeteuliwa kushika nafasi ya Mbunge Dk Elly Macha amefuata nyayo za Mama Salma Kikwete baada ya kuuliza swali mara baada ya kumaliza kuapishwa.

Katika swali lake la nyongeza kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mbunge huyo alitaka kufahamu mkakati wa Serikali katika kuutangaza Ukanda wa Magharibi wa Utalii wa mkoani Mara katika kuongeza utalii.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani alisema, “Katika Western Corridor (Ukanda wa Magharibi wa Utalii) ikiwemo Ziwa Victoria, kunapopakana na Mbunga ya Serengeti, Serikali imeshaweka mipango ya kuuboresha ukanda huo mfano mageti ya kuingia Serengeti sasa yatakuwepo upande wa Mara na Shinyanga na haitakuwa Arusha pekee”.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Chambani, Yussuf Salim Hussein (CUF) alitaka kufahamu serikali ilivyojipanga kukakabiliana na ongezeko la uwekezaji katika sekta ya utalii.

Makani alisema mambo yanayochangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa utalii ni ujenzi wa barabara na viwanja vya ndege uliokamilika na unaoendelea, ununuzi wa ndegembili uliokamilika na nyingine nne zinazotarajiwa kuja nchini katika siku za karibuni.

Alisema ili kufanya ongezeko hilo liwe na tija na endelevu, Wizara ya Maliasili na Utalii imejikita katika kusimamia ubora wa huduma na utoaji wa huduma na kutangaza zaidi vivutio hususan vivutio vipya.

Nyingine ni kusambaza shughuli za utalii nchi hususan Ukanda wa Kusini ili kutimiza azma ya Serikali kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano wa Mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021 unaoainisha utanuaji wa uwigo wa mazao ya utalii kama mojawapo ya hatua muhimu za kuchukua ‘key interventions’ katika kukuza utalii nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *