Mahakama ya Hakimu ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewapatia dhamana viongozi sita wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), bila washtakiwa hao kuwapo mahakamani huku wakitakiwa kuripoti kila Alhamisi.
Awali, viongozi hao akiwamo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, walidhaniwa kuletwa mahakamani hapo na mahakama ikaamua kuketi na mawakili wa pande zote mbili kujadili kama washtakiwa hao wataletwa au la ili itoe uamuzi wake.
Baada ya makubalianao hayo, Inspekta Shabani wa Magereza ameieleza mahakama kuwa washtakiwa hao wameshindwa kuletwa mahakamani hapo kwa sababu gari la kuwaleta ni bovu.
Akitoa uamuzi wake, Hakimu Mkazi Wilbard Mashauri amewataka washtakiwa hao kuwa na wadhamini wawili kila mmoja na kusaini kwa maandishi ya Sh milioni 20.
Baada ya maamuzi hayo,Wakili wa serikali, Faraja Nchimbi ameieleza Mahakama kuwa wataka rufaa kupinga uamuzi wa mahakama hiyo kutoa masharti ya dhamana kwa Mbowe na wenzake.
Pamoja na Mbowe, viongozi wengine ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko ambao wanakabiliwa na mashtaka manane yakiwamo kuhamasisha maandamano, uchochezi na uasi.