Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wengine wachama hicho wameachiwa kwa dhamana baada ya kuhojiwa Kituo Kikuu cha Polisi.

Viongozi hao walikwenda kituoni hapo baada ya Mbowe kumaliza mkutano wake na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho yaliyopo mtaa wa Ufipa, Kinondoni.

Februari 20, 2018 Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam iliagiza kukamatwa viongozi saba waandamizi wa Chadema akiwamo Mbowe.

Wito huo ulikuja siku chache baada ya tukio la kuuawa kwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.

Akwilina aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni jijini Dar es Salaam wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakienda ofisi za mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kudai viapo kwa mawakala wao.

Viongozi wengine waliohojiwa sambamba na Mbowe ni  naibu makatibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).

Pia, wamo mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee; mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, John Heche na Esther Matiko ambaye ni mweka hazina wa Bawacha.

Mdee, Matiko, Heche na Mnyika walisharipoti awali na walitakiwa kurejea kituoni leo. Viongozi wengine waliwakilishwa na wanasheria.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji  hakwenda polisi kwa kuwa yupo nje ya nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *