Mwenyekiti wa chadema, Freeman Mbowe amesema bado hawajafahamu ni taratibu gani zimetumika kuwaachia huru wakati kifungo chao kilikuwa bado.
Mbowe amesema kuwa katika mazingira ya kawaida, siku yao ya kifungo walichokuwa wamepewa kilikuwa kinaishia Juni 5, mwaka huu, lakini ghafla wakapewa taarifa kwamba wataachiwa leo.
Pia Mbowe amesema kuwa tangu wamewekwa gerezani ni takribani miezi mitatu, mawakili wao walifanya jitihada za kuhakikisha rufaa yao katika mazingira ya dharura inasikilizwa, lakini haikuwahi kupata jaji wala kusikilizwa kwa sababu kila jaji aliyepangiwa kesi hiyo alionekana ana udhuru.
Aidha amesema wao wanaamini kesi hiyo haikuwa ya haki kwa sababu watuhumiwa walinyimwa dhamana mwanzoni, na kutokana na mazingira ya kesi yenyewe hawakutakiwa kupewa kifungo. Pia amedai kwamba wataendelea na rufaa yao ili kuweka rekodi sawa na kudhihirisha kwamba Sugu na Masonga hawakuwa na makosa.
Sugu na Masonga walitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miezi mitano jela Februari 26 mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya kwa kutoa lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli kwenye mkutano wa hadhara walioufanya Desemba 30 mwaka jana eneo la Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.