Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amesema kuwa ameshangazwa na kitendo cha Rais Magufuli kutomuwajibisha mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda anyetuhumiwa kuvunja sheria na kumvua uwaziri Nape kutokana na kosa la mteule.

Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa Chadema amesema hayo jana wakati akiwasilisha maoni ya kambi ya upinzani kuhusu bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake kwa mwaka 2017/18.

Mbunge huyo wa Hai amesema kuwa kambi ya upinzani imeshangazwa na kitendo cha Rais Magufuli kuendelea kumkingia kifua mkuu wa mkoa huyo katika matukio tofauti ambayo ushahidi wa wazi wa matumizi mabaya ya madaraka na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Mbowe amezitaja baadhi ya tuhuma za mkuu wa mkoa huyo ni utajiri wake wa ghafla na kutumia magari ya kifahari ya watu waliohusika na tuhuma za madawa ya kulevya.

Pia Mbowe ameongeza tuhuma zingine ni kuvamia kituo cha TV cha Clouds Media akiwa na askari wenye silaha za moto mwezi uliopita.

Mbowe amesema kuwa kutokana na hayo Serikali ya awamu ya Tano imeonyesha dalili za wazi za kuvunja katiba na kutupilia mbali misingi ya misingi ya utawala wa sheria, demokrasia na uhuru wa habari.

Source: Mwananchi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *