Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amepewa siku 14 na serikali awe amelipa kodi ya hoteli yake ya Aishi takribani milioni 13.5 vingine vyo hoteli hiyo itafungwa.
Hoteli ya Aishi inayomilikiwa na Freeman Mbowe iliyopo Machame wilayani Hai mkoani Kilimanjaro ipo mbioni kufungiwa kutokana na deni hilo.
Uamuzi huu wa serikali ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro umekuja siku moja tangu Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gellasius Byakanwa alipotangaza kusitisha shughuli za kilimo katika shamba la Kilimanjaro Veggies linalomilikiwa na Mbowe kwa madai kuwa lipo katika eneo la chanzo cha maji cha Mto Weruweru.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa mujibu wa taarifa alizozipata kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Freeman Mbowe amekuwa akikwepa kulipa kodi kwa miaka mitano na kusababisha halmashauri kushindwa kufikia malengo ya ukusanyaji mapato.
Kwa miaka mitano imeelezwa kuwa Mbowe hakupeleka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hali ya mauzo yake ambayo inapaswa kutumika kujua ni kodi kiasi gani anatakiwa kulipa.
Source: Global Publishers