Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kimesikitishwa na hatua ya uongozi wa Bunge la Tanzania ya kulichukua gari la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni (KUB), Freeman Mbowe alilokuwa akilitumika kwa shughuli za matibabu ya Tundu Lissu jijini Nairobi.
Chadema imesema Mbowe ambaye ni Mbunge wa Hai, aliamuru gari hilo lipelekwe Nairobi kwa ajili ya kusaidia matibabu ya Lissu ambaye ni mwanasheria mkuu wa chama hicho
Lissu ambaye pia Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alishambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Septemba 7 akiwa nyumbani kwake Area D mjini Dodoma na yuko Nairobi kwa matibabu.
Mkuu wa Idara ya Uenezi Chadema, Hemed Ali ameeleza hayo leo Alhamisi wakati akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu na kwamba hawana wasiwasi na hatua hiyo kwa kuwa wana marafiki wengi wakiwamo Watanzania waishio nchini humo na Wakenya wenyewe ambao kwa namna moja au nyingine watashirikiana nao.
Akizungumzia suala hilo Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah amedai kuwa hana na taarifa hizo, ndiyo kwanza anazisikia kutoka kwa mwandishi na alimtaka mwandishi amuulize huyo aliyetoa taarifa kama kweli ametumwa na Mbowe.