Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameitaka Serikali kudhibiti matukio ya watu kuuawa kikatili nchini.
Akizungumza jana wakati wa kuaga mwili wa aliyekuwa Diwani wa Namwawala wilayani Kilombero, Godfrey Luena aliyeuawa Februari 22 kwa kukatwa mapanga, Mbowe alisema Watanzania wasikubali kuingia katika uadui wa kisiasa.
Mbowe alisema matukio yanayotokea sasa ya mauaji yanatia shaka na Serikali isipoyadhibiti itasababisha wananchi wanaopotelewa na ndugu kukaa na manung’uniko.
Alimuomba Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, James Ihunyo aliyehudhuria mazishi hayo kuwatuliza vijana wenye jazba kuhusu matukio yanayoendelea nchini. Mkuu wa Wilaya, Ihunyo aliposimama kuzungumza alisema wameshaunda timu maalumu kuwasaka waliohusika na tukio hilo.
Awali, Mbowe alisema matukio ya mauaji ya kikatili dhidi ya viongozi wa Chadema hayatairudisha nyuma badala yake wataendelea kuimarika.
Alisema kwa kuwa Polisi imetoa tamko kuwa kushambuliwa Luena kunatokana na kisasi, hivyo inawajua watuhumiwa, ana imani watakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya dola.