Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amesema kuwa baadhi ya madiwani wa CHADEMA ambao wanajiuzulu nafasi zao wananunuliwa na Wakuu wa Wilaya.
Mbowe amesema hayo alipokuwa kwenye mkutano wa hadhara katika ziara yake jimboni Hai mkoani Kilimanjaro, ambapo alikuwa katika kijiji cha Kyuu na kusema kuwa kitendo cha kuwanunua madiwani hao wa CHADEMA ni kupoteza fedha za Umma tu.
“Kwanza ninawashukuru sana wakazi wa Masama Mashari kwa kura nyingi mlizotupatia na ni wajibu wetu kuwatumikia nyinyi, ila nataka niwaeleze jambo moja hii biashara ya kununua Madiwani inayofanywa na Mkuu wa Wilaya, tunamwambia Rais ni matumizi mabaya ya fedha za umma kurudia uchaguzi”.
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepata pigo Kanda ya Kaskazini kutokana na ukweli kwamba zaidi ya madiwani 10 waliamua kujiuzulu nafasi zao kama madiwani na wengine kutangaza kumuunga mkono Rais John Pombe Magufuli na serikali yake.