Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZPC), Kamishna Simon Sirro na Mkuu wa Upelelezi wa kanda hiyo (ZCO), Camilius Wambura, wamepelekewa barua za mwito za kuwataka wafike Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo.

Viongozi hao wamepelekewa mwito huo kutokana na kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe dhidi yao.

Mbowe amefungua kesi hiyo kupinga Makonda kumtaja katika orodha yake ya watuhumiwa 65 wanaojihusisha na dawa za kulevya katika awamu ya pili na kumtaka afike katika Kituo Kikuu cha Polisi, Februari 10 mwaka huu, kwa ajili ya mahojiano.

Katika kesi hiyo Namba Moja ya Mwaka 2017, Mbowe pamoja na mambo mengine, anapinga mamlaka ya RC kumkamata kwa kile anachokiita kudhalilisha watu.

Kesi hiyo imepangwa kutajwa leo na itasikilizwa na jopo la majaji watatu, Sekieti Kihiyo ambaye ni kiongozi wa jopo hilo, akisaidiana na Jaji Lugano Mwandambo na Jaji Pellagia Kaday.

Mbowe anaiomba mahakama hiyo itamke kuwa vifungu vya Sheria ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa vinavyowapa mamlaka wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuwakamata watu na kuwatia mbaroni viko kinyume cha Katiba.

Aidha, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, jana alifungua maombi mahakamani hapo akipinga kusudio la Kamanda Sirro la kumkamata kama hatajisalimisha katika kituo cha polisi kwa mahojiano.

Mahakama hiyo imetoa hati za mwito wa kufika mahakamani hapo kwa wadaiwa hao ambao ni Makonda, Sirro na Wambura. Hata hivyo, inadaiwa Kamanda Sirro alikataa kupokea mwito huo akielekeza kuwa hati hiyo ya mwito ipelekwe kwa Wambura.

Wadaiwa kukataa kusaini Kwa mujibu wa Ofisa wa mahakama, Yusuph Juma ambaye alipeleka mwito huo, alidai kuwa baada ya kuelekezwa na Kamanda Sirro kuwa ampelekee mwito huo Wambura, alipokwenda kwa Wambura, hakumkuta.

Juma alidai hati ya mwito wa mkuu wa mkoa alipoupeleka hakumkuta na kwamba wasaidizi wake nao walikataa kuusaini mwito huo.

Source: Habari Leo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *