Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Amos Makalla ameagiza kusimamishwa ujenzi wa vibanda na vyoo uliokuwa ukifanywa na wafanyabiashara katika soko la Uhindini mkoani humo.
Uhamuzi huo ameutoa baada ya mkurugenzi wa jiji la Mbeya, Nachoa Zacharia na Ofisa ardhi, Jacob Ngowi kukana kutambua ujenzi wa majengo unaoendelea baada ya Makalla kuwaruhusu wafanyabiashara kujenga vibanda vya muda.
Februari 2 mwaka huu, mkuu wa mkoa huyo aliwarejesha wafanyabiashara 459 sokoni hapo na kuwaruhusu kujenga vibanda vya muda vya biashara huku akisema uongozi wa jiji umeshindwa kuvijenga.
Kwenye mkutano na wafanyabiashara hao, Makalla amesema kuwa alibaini baadhi ya viongozi walitaka kubadili matumizi ya eneo hilo kwa kuweka mradi wa maegesho ya magari jambo ambalo serikali imelipinga.
Baada ya kauli hiyo wafanyabiashara wakaanza kujenga vibanda lakini mkuu wa mkoa alisitisha baada ya ofisa mipango wa miji mstaafu, Prince Mwaihojo kuishauri Serikali kutafuta wawekezaji na kuangalia sera ya mipango miji katika ujenzi wa vibanda vya wafanyabiashara ndani ya soko hilo.