Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limedai kuwa waasi kwenye Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) limewaua raia 32 mwezi Disemba mwaka jana.

Shirika la Human Rights Watch limedai kuwa wanajeshi wa kundi la ‘The Union for Peace in the Central African Republic (UPC)’ liliwazingira wahanga hao kisha kuwaua kwasababu za tofauti za kisiasa.

HRW limedai kuwa linahofia vikosi vya kulinda amani nchini humo vya Umoja wa Mataifa vinaweza kushindwa kukabiliana na hali ya mauaji hayo.

UPC ni sehemu iliyojitenga kutoka katika kundi la Seleka ambalo lilotwaa madaraka ya nchi hiyo kwa muda mfupi mwaka 2013.

Wapiganaji hao wa UPC wanadaiwa kuwaua watu 25 kwenye mji wa Bakala mnamo tarehe 12 Disemba baada ya kuwaita shuleni kwaajili ya mkutano.

HRW limedai kuwa kabla ya kuwaua watu hao 25 tayari lilishawaua watu 7 waliokuwa wanatokea kwenye mgodi wa dhahabu uliopo karibu na maeneo hayo.

Wakati huo huo, wanajeshi wa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa (UN) wamekuwa wakituhumiwa kuwanyanyasa kijinsia watoto na baadhi ya raia wa Afrika ya Kati wamekuwa wakiwataka wanajeshi hao kuondoka kwa kushindwa kuwalinda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *