Taassi ya tiba ya mifupa Muhimbili (MOI) imesema kuwa Bondia Mohamed Matumla amefanyiwa upasuaji wa kichwa na anatarajia kurejea kwenye hali yake ya kawaida kwa kipindi cha miezi nane hadi 12.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo Othmani Kiloloma amesema baada ya kumpokea bondia huyo walimfanyia uchunguzi wa kina na kugundua kuwa amepata athari katika ubongo hivyo wakalazimika kumfanyia upasuaji ili kuweza kuokoa maisha yake.
Kiloloma amesema, upasuaji ulifanyika kwa mafanikio makubwa chini ya jopo la wataalam wazalendo watano kwa muda wa masaa matatu huku akiongeza kuwa mara baada ya upasuaji huo bondia huyo kwa sasa anaendelea vizuri na matababu.
Kwa upande wake Katibu wa Kamisheni ya mchezo wa ngumi za kulipwa Tanzania TPBC Chacha Michael amesema, Matumla alishindwa kuendelea na mpambano usio na ubingwa katika mzunguko wa saba lakini walifanikiwa kumuwahisha hospitali ambapo alifanyiwa upasuaji na sasa anaendelea na matibabu ili kuhakikisha anarudi katika hali yake ya kawaida.
Bondia huyo amefanyiwa upasuaji wa kichwa kutokana na maumivu aliyoyapata baada ya kupigwa na Bondia Mfaume Mfaume katika pambano lisilo la ubingwa.