Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya mitihani ya upimaji wa darasa nne na kidato cha pili iliyofanyika Novemba 22 na 23 mwaka jana, huku idadi kubwa ya wanafunzi wakifanya vyema katika mitihani hiyo.
Akitangaza matokeo hayo leo Jumatatu Januari 8, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde amesema jumla ya wanafunzi 1,086,156 waliofanya mtihani wa darasa la nne wamefaulu kati ya 1,158,444 waliofanya upimaji huo.
Amesema wanafunzi hao wamefaulu kwa kupata alama zenye madaraja ya A,B,C na D wakati wanafunzi 72,288 sawa na asilimilia 6.24 wamepata alama za daraja E, ambao ni ufaulu usioridhisha.
Kuhusu matokea ya upimaji wa kidato cha pili, Dk Msonde amesema jumla ya wanafunzi 433,453 sawa na asilimia 82.32 kati ya 486,742 waliosajiliwa kufanya mtihani huo wamepata ujuzi wa maarifa ya kuwawezesha kuendelea na kidato cha tatu.
Dk Msonde alisema wanafunzi wa kidato cha pili 51,807 sawa na asilimia 10.68 wameshindwa kupata alama za kuwawezesha kuendelea na kidato cha tatu.