Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Hamadi Masauni anatarajia kuongoza kampeni ya kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika kukabiliana na ajali Tanzania unaolenga kupunguza ajali hasa kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa mwaka ambapo watu wengi husafiri.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya RSA Tanzania, Jackson Kalikumtima alisema kuwa kampeni hiyo ni muda wa miezi sita na hasa italenga namna ya kukabiliana na ajali kwa kuchukua hatua stahiki bila ya kuwepo askari.
Amesema baada ya kufanyika uzinduzi wa kampeni hiyo hapo kesho, mabalozi wa usalama barabarani waliotawanyika kote nchini kwa kushirikiana na askari wa usalama barabarani, Sumatra na Chama Cha Kutetea Abiria (Chakua) na vyama vingine wataenda kwenye vituo vya mabasi, vyuoni, shuleni na kwa waendesha pikipiki kwa lengo la kutoa elimu juu ya usalama wa abiria katika chombo cha kusafiria na tahadhari yake.
Kwa upande wake Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, DCP Mohamed Mpinga alisema kuwa anawaomba wananchi kuunga mkono juhudi zinazofanywa na vyama hivi au taasisi za kuangalia usalama wa abiria na kutoa taarifa mara moja wawapo kwenye chombo cha moto.