Mwili wa Meya wa zamani wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi, leo utaagwa na viongozi wa kitaifa pamoja na wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kwenye Viwanja vya Karimjee, kabla ya kwenda kuzikwa katika Chuo cha ugavi na ununuzi cha IPS kilichoko Chanika wilaya ya Ilala.
Msemaji wa familia, Edson Fungo amesema kwa kuwa Dk Masaburi alikuwa mwanasiasa na amewahi kushika nyadhifa mbalimbali kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikalini, familia imeona vyema watoe fursa ya kuagwa na wanasiasa wenzake pamoja na wakazi wa jiji la Dar es Salaam.
Dk Masaburi kabla ya kuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam aliwahi kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki.
Wakati akiwa Meya alichaguliwa pia kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALART).
Hadi mauti yanamkuta, Dk Masaburi alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana wa Chuo cha IPS kilichoko Chanika nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Dk Masaburi aliaga dunia usiku wa kuamkia Alhamisi wiki iliyopita katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako alikuwa amelazwa akisumbuliwa na homa ya Ini (Hepatitis B).