Mmiliki wa Facebook, Mark Zuckerberg amewaambia maseneta wa Marekani kuwa kampuni yake imekuwa ikipambana na watumiaji wa Warusi wanaotaka kuutumia vibaya mtandao huo wa kijamii.
Bw Zuckerberg alikua akijibu maswali kuhusiana na sakata ya matumizi mabaya ya data za kibinafsi maarufu kama Cambridge Analytica.
Pia amefichua kuwa Robert Mueller, kutoka baraza maalum linalochunguza madai ya Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani wa Mwaka 2016 aliwahoji wafanyakazi wa Facebook.
Mwezi Februari, Ofisi ya Bw Mueller ilishtakiwa na Warusi 13 kwa kudukua taarifa za uchaguzi wa mwaka 2016, pamoja na makampuni matatu ya Urusi.
Bw Zuckerberg amesema kuwa kampuni yake sasa imetengeneza nyenzo za kubaini akaunti gushi.
Awali Mtendaji mkuu wa mtandao wa kijamii Facebook, Mark Zuckerberg ameomba msamaha kwa kamati ya Seneti ya Marekani kwa kuruhusu makampuni kadhaa kutumia vibaya data binafsi za jukwaa hilo kisiasa.
Mark Zuckerberg alijitetea kwa muda wa saa tano katika jopo la wasikilizaji kutoka bunge la seneti la Marekani linalohusika na masuala ya biashara na kamati ya mahakama.