Nchi ya Marekani imemtaka kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga kuacha mpango wake wa kuapishwa kama rais wa nchi hiyo wiki ijayo.
Odinga aliwasilisha kesi juu ya mapungufu katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 8 Agosti katika Mahakama ya Juu nchini humo ambayo ilibatilisha uchaguzi huo na kuagiza uchaguzi wa marudio ufanyike.
Odinga na muungano wake wa National Super Alliance hata hivyo walisusia uchaguzi huo wa 26 Oktoba ambapo rais Kenyatta alitangazwa mshindi na mwishowe kuapishwa kwa muhula wa pili.
Waziri msaidizi wa Marekani kuhusu masuala ya Afrika, Donald Yamamoto ambaye alikuwa amezuru Kenya alimtahadharisha Bw Odinga na pia akahimiza kuwepo mashauriano kati yake na serikali iliyopo madarakani.
Baadhi ya viongozi wa serikali wameonya kuwa tukio hilo la kuapishwa linaweza kuhusishwa na uhaini.
Mshauri wa Bw Odinga Salim Lone alipuuzilia mbali onyo hilo la Marekani na kusema Bw Odinga ataapishwa kama ilivyopangwa Jumanne wiki ijayo.