Marekani ,Uingereza na Ufaransa zimeanza mashambulizi ya anga ya pamoja dhidi ya silaha za kemikali za Assad  nchini Syria.

Hii ni baada ya serikali ya Assad kufanya shambulizi baya la kemikali dhidi ya raia na kusababisha vifo vya watu zaidi ya sabini huku wengine wengi wakiwa wamejeruhiwa.

Waziri wa ulinzi wa Marekani James Mattis amesema kuwa nchi hizo tatu zimechagua silaha muhimu kwa ajili ya shambulizi hilo na anaamini shambulizi hilo ni kali ukilinganisha na mashambulizi yaliyofanywa hapo awali.

Kamanda wa majeshi wa Marekani Jenerali Joseph Dunford amesema kuwa Urusi haikupewa taarifa kuhusu shambulizi hilo.

Naye rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameituhumu serikali ya Assad na kusema kuwa shambulizi lililofanywa dhidi ya raia haliwezi kusameheka na kwamba ilikuwa hamna namna ya kumdhibiti Assad zaidi ya kutumia nguvu.

Naye rais wa Marekani Donald Trump amezidi kulikemea shambulizi hilo na kusema kuwa limeacha binadamu katika hali mbaya na maumivu makali.Anaamini aliyefanya shambulizi hilo hawezi kuwa binadamu bali ni mnyama.

Trump amehakikisha kuwa nchi hizo tatu kwa pamoja zitaendeleza mashambulizi mpaka pale jeshi la Assad litakapoacha mashambulizi yake.

Nchi hizo tatu vilevile zinatarajia kuibana Syria kidiplomasia na kiuchumi kama moja ya hatua ya kupinga shambulizi lililofanywa na Assad.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *