Maofisa watano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wanaotuhumiwa kushiriki kumwondoa faru John kutoka katika Creta hiyo wamekamatwa juzi kwa mahojiano ili kujua ukweli kuhusu mazingira ya kupotea kwake.
Hatua ya maofisa hao kukamatwa imekuja siku tatu baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuituhumu menejimenti, wafanyakazi wa NCAA na Baraza la Wafugaji (NPC) kuwa imejaa vitendo vya rushwa na wizi na asingeweza kuvumilia sakata la faru John ambaye alisema kuwa aliuzwa kwa Sh200 milioni kwenye Hoteli ya Grumet iliyo Hifadhi ya Serengeti na kuwa walipokea fedha za awali Sh100 milioni.
Waziri Mkuu alisema anataka kumwona faru huyo, nyaraka za kumhamisha na kama amekufa basi apelekewe hata pembe ofisini kwa kuwa anajua pa kuzipeleka.
Habari za uhakika kutoka Ngorongoro, ambazo zimethibitishwa na Jeshi la Polisi zinasema kuwa maofisa hao watano wanashikiliwa katika kituo chao cha Ngorongoro kutokana na ushiriki wao kwa njia moja au nyingine.
Wanaoshikiliwa ni pamoja na Israel Naman ambaye alikuwa Kaimu mkuu wa idara ya uhifadhi wakati faru huyo akiondolewa.
Wengine ni Cuthbert Lemanya, ambaye alikuwa Mkuu wa Kanda ya Creta, Dk Athanas Nyaki ambaye anadaiwa kumdunga sindano ya usingizi ili aweze kubebwa.