Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji amekabidhi eneo litakalojengwa uwanja wa klabu hiyo ufukweni mwa bahari ya Hindi, Gezaulole, Kigamboni.
Wasaidizi wa Manji wamekabidhi eneo hilo jana mchana katika hafla fupi iliyohudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba na maofisa wa serikali ya Kigamboni.
Mwenyekiti wa baraza la wadhamini wa Yanga, Fatma Karume ndiye aliyepokea eneo hilo kwa niaba ya klabu ambapo pia walikuwepo Dk Jabir Katundu, ambaye ni mjumbe wa baraza la wadhamini, mjumbe wa kamati ya utendaji ya Yanga, Samuel Lukumay na Katibu Mkuu, Baraka Deusdedit.
Manji amekabidhi eneo hilo ikiwa ana hesabu kadhaa zilizosalia kabla hajakabidhiwa timu baada ya mechi ya keshokutwa.
Baada ya kukabidhiwa eneo hilo, wadhamini wa klabu hiyo wanatarajia kulitambulisha rasmi kwa wanachama wao wiki ijayo. Eneo hilo lina ekari 715 ikiwa ni ukubwa zaidi ya eneo lililojenga Uwanja wa Uhuru.
Tayari Yanga ina ramani tatu za uwanja mkononi ilizokabidhiwa mwaka jana na Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group (T) Ltd (BCEG) ya China ambao utachukua miaka miwili kukamilika.
Gharama za ujenzi wa uwanja namba moja ‘A’ ni dola za Marekani milioni 50, pamoja na ofisi, ukumbi wa mikutano, maduka, maegesho ya magari na sehemu ya mazoezi (gym).
Kwa mujibu wa ramani hizo, Uwanja A ambao ni wa kufunikwa juu, utakuwa na uwezo wa kubeba watazamaji 50,000, kama ulivyo Uwanja B utakaochukua watazamaji 40,000, wakati Uwanja C utakaokuwa umefunikwa jukwaa kuu pekee utaingiza watazamaji 30,000 walioketi.
Yanga imeamua kuchukua eneo Gezaulole baada ya kukataliwa kupewa eneo la nyongeza Jangwani kutokana na eneo hilo kuwa hatarishi kwa vile ni mkondo wa maji.