Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, IGP Mstaafu Ernest Mangu amemuahidi Rais Dkt. Magufuli kwamba atahakikisha anadumisha mahusiano mazuri baina ya Rwanda na Tanzania ili kuweza kuipeleka nchi katika maendeleo mazuri ya kiuchumi.
Balozi Mangu ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa anatoa salamu zake kwa Rais Magufuli pamoja na viongozi wengine walihudhuria hafla hiyo Ikulu Jijini Dar es Salaam ya kula kiapo cha Utii ili kuweza kutumika nafasi aliyoteuliwa.
“Nimefarijika sana kuona Rais Magufuli bado unaendelea kunikumbuka na kuona bado naendelea kufaa kutumika chini yako. Ninachokuahidi kwamba nitaendelea kuwa muaminifu, ntatumia nguvu na akili zangu zote kuhakikisha kwamba natekereza majukumu ya kibalozi kama ambavyo yameanishwa kwenye sheria na taratibu mbalimbali”, amesema Balozi Mangu.
Pamoja na hayo, Balozi Ernest Mangu ameendelea kwa kusema “naelewa umuhimu wa nchi ya Rwanda kwa maendeleo ya uchumi wa nchi yetu na hasa katika sekta ya bandari, usafirishaji na masuala mazima ya uhusiano ya kimataifa hivyo naahidi nitaenda kufuatilia mambo yote hayo ili kuweza kudumisha uhusiano wetu na nchi za jirani”.
Kwa upande mwingine, Makamu wa Rais Samia Suluhu amempongeza Balozi Ernest Mangu wa Tanzania nchini Rwanda, na Meja Jenerali Mstaafu Simon Marco Mumwi wa Urusi kwa kuweza kula kiapo siku ya leo (Machi 21, 2018) na kuwataka wakabiliane na kazi nzito iliyokuwa mbele yao ili kuweza kuileta matunda mazuri nchi yao Tanzania kwa kile watakachokifanya huko.