Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amefunguka mambo ambayo yanaendelea nchini hivi sasa na kusema serikali ya CCM inahangaika kuhamisha mjadala wa watu ambao wameshambulia Tundu Lissu.
Zitto Kabwe amesema kuwa jana alipoona picha za Tundu Lissu na kusikia sauti yake alifarijika kwani sasa anaamini kuwa kiongozi huyo siku za karibuni ataungana na wao katika kuendelea kupambana kujenga Demokrasia ya nchi.
Aidha Mbunge huyo amedai kuwa kitendo cha madiwani kununuliwa na viongozi wengine wa upinzani ni ajenda ya serikali ya CCM kuhakikisha wanazima mazungumzo juu ya watu ambao walifanya shambulio kwa lengo la kutaka kumuuwa Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu.
“Yote hayo yanayoendelea, CCM inafanya juhudi kubwa kuhamisha mjadala kuhusu waliokushambulia kwa kununua madiwani na wanachama wa vyama vya upinzani kila siku, wakiubana zaidi Uhuru wa habari, na wakiuzima uhuru wa vyama vya siasa, hawataki kabisa mawazo mbadala ya kututoa katika hali tuliyonayo. Utakaporudi naamini utakuta mengine mengi mapya. Ninafuraha kuwa unaendelea vizuri sana tofauti na nilipokuja kukuona. Tutazidi kumwomba Mola afya yako iimarike zaidi. Tuna kazi kubwa sana mbele ya safari, na kwa hakika ni lazima tuifanye kwani tusipoifanya Nchi yetu itaanguka Kiuchumi na Kidemokrasia, na watu wetu kuendelea kuwa masikini zaidi kuliko ilivyo sasa”.
Pia ameendelea kuandika “Mbali na hilo Zitto Kabwe aliendelea kusema “Kupigwa risasi wewe ilikuwa ni lengo la waliokushambulia kutunyamazisha. Tumewaambia kuwa hatutanyamaza kamwe. Kama ulivyoniambia ukiwa kitandani kuwa “tumeshashinda. Tutashinda”. Hakika ushindi ni dhahiri na ndio maana wanatapatapa kuzuia Uhuru wa mawazo na fikra. Lakini Shambulio la kutaka kukuua limetuonyesha watu wanaoumizwa na ‘INJUSTICE’ na wasioumizwa nayo. Wengi wasioumizwa na ‘Injustice’ wanadiriki hata kuhoji kwanini eti tunapaza sauti kuhusu suala lako”.
Zitto Kabwe ni kati ya Wabunge ambao waliweza kufika jijini Nairobi kwenda kumjulia hali Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu wiki kadhaa zilizopita.