Waziri wa elimu nchini Sweden, Aida Hadzialic amejiuzulu wadhifa wake baada ya kupatikana na hatia ya kuendesha gari huku akiwa amelewa.
Bi Aida Hadzialic, ambaye ni waziri wa elimu ya sekondari na elimu ya watu wazima, amejiuzulu baada ya kukamatwa na polisi mjini Malmo nchini humo.
Waziri huyo ndiye waziri mdogo zaidi kuwahi kuteuliwa nchini humo amesema kwamba sharti awajibike kwasaababu ni kosa kubwa zaidi alilowahi kulifanya maishani mwake.
Bi Aida Hadzialic alipimwa na kugunduliwa kwamba alikuwa amepitisha kidogo kipimo kinachoruhusiwa cha unywaji pombe.
Nchi ya Sweden huwa na sheria kali sana za kuzuia uendeshaji gari mtu akiwa amelewa.
Bi Hadzialic alihamia Sweden kama mkimbizi kutoka Bosnia Herzegovina akiwa mdogo, amesema alikuwa amekunywa gilasi mbili pekee za mvinyo.