Mali za kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd iliyotajwa katika sakata la zabuni ya Sh34 bilioni ya kuweka mashine za kielektroniki za kuchukua alama za vidole ya Jeshi la Polisi zinatarajiwa kupigwa mnada kutokana na kudaiwa kodi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mnada wa maghorofa hayo utafanywa na kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart, kwa niaba ya TRA Mkoa wa Ilala.

Maghorofa hayo yapo maeneo tofauti jijini Dar es Salaam; moja Mtaa wa Mazengo, Upanga na mawili yako Mbweni JKT wilayani Kinondoni.

Mkurugenzi mtendaji wa Yono, Scolastica Kevela amesema mnada huo utafanyika Septemba 9, kuanzia saa 4:30 asubuhi kwenye maeneo yalipo maghorofa hayo.

Kevela amesema Lugumi Enterprises imeshindwa kulipa kodi ya TRA kwa wakati ndiyo maana wakapewa kazi ya kuuza majengo hayo.

Mkurugenzi huyo alikataa kutaja kiasi ambacho Lugumi anadaiwa na TRA pamoja na thamani ya maghorofa hayo.

Kevela alitoa rai kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kulipa kodi kwa wakati ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, masharti ya mnada ni kulipa asilimia 25 ya thamani ya bei kwa atakayefanikiwa kuyanunua maghorofa hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *