Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imekamata makontena 262 yenye mchanga wa dhahabu yaliyokuwa yamehifadhiwa katika bandari kavu ya MOFED (zamani ZAMCARGO) iliyopo Kurasini jijini Dar es salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko, amesema makontena hayo yaliyokuwa katika hatua za mwisho kukamilisha taratibu za kiforodha yamebainika leo tarehe 25 Machi, 2017 katika msako mkali unaoendeshwa na Mamlaka yake.

Mhandisi Kakoko amesema makontena yote hayo yalikuwa na lakiri (seals) za Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), na yalikuwa yanashughulikiwa na kampuni ya usafirishaji wa mizigo ya Freight Forwarders Tanzania Limited iliyopo Dar es salaam.

Mhandisi Kakoko amesema jumla ya makontena 256 yalikuwa katika bandari kavu ya MOFED, wakati makontena mengine sita yalikuwa tayari yameshaingizwa bandarini tayari kwa kusafirishwa.

Ametoa wito kwa makampuni yote ya madini yenye shehena za mchanga yajitokeze yenyewe na kuonesha mizigo yao popote ilipo nchini kabla haijabainika katika msako kabambe unaondeshwa na vyombo vya ulinzi na usalama katika maeneo mbalimbali nchi nzima.

Orodha ya makontena hayo yaliyobainika inaonesha yalifika bandarini hapo katika nyakati tofauti kutoka migodi ya Buzwagi na Pange Mines.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *