Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage ametoa siku nne kwa wafanyabiashara waliopitisha makontena 100 bandarini bila kukaguliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), wakatoe taarifa katika shirika.
Mwijage alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupata taarifa kuwepo kwa makontena 100, yaliyotolewa bandarini kwa siku zilizopita bila kukaguliwa na TBS.
Alisema wafanyabiashara ambao hawatajisalimisha baada ya kumalizika kwa siku hizo, hatua stahiki zitachukuliwa ikiwemo kulipa faini ya asilimia 15.
Aidha, alisema kwa mawakala wa forodha wote, waliohusika kutoa kontena hizo wizara yake itawasiliana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ili kuona hatua za kuchukua kwa kuwa serikali haiwezi kukubali mchezo huo.
Pia alisema kontena hizo zilipaswa kukaguliwa na TBS, lakini baada ya tukio hilo kontena hizo zitakaguliwa na shirika hilo wakishirikiana na Tume ya Ushindani Tanzania (FCC). Aidha, amewaagiza TBS na FCC wafuatilie watu wao na kuziona bidhaa hizo, kwani watakaoshindwa hawatapewa cheti cha ubora bila kuona bidhaa na kukaguliwa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk Egid Mubofu alisema ni vyema wafanyabiashara hao wakafuata maagizo hayo na kujitokeza kukaguliwa ilikuepuka faini hiyo ya asilimia 15. Alisema upitishaji wa bidhaa bila kukaguliwa na shirika hilo unaweza kuleta madhara makubwa kwa watumiaji ambao hawajui kama bidhaa yako imekaguliwa ubora.
TBS imeanzisha utaratibu mpya wa kulipisha faini mizigo inayoingia hapa nchini, ambayo haikukaguliwa wakati iko nchini China. Faini ni asilimia 15 ya thamani ya mzigo ulioingia.