Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amezindua ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa moja kutoka eneo la Shimo la Udongo Kurasini hadi Polisi Ufundi.

Barabara hiyo inajengwa na Kampuni ya kitanzania ya Grand Tech, ambayo imejitolea kwa gharama zake itajengwa kwa kiwango cha zege yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 700.

Makonda amesema kampuni hiyo imeamua kujitolea kufanya ujenzi wa barabara hiyo baada ya kusikia jitihada za wadau kutoa michango mbalimbali katika kuendeleza jiji hilo.

Vile vile Makonda alisema baada ya wadau hao, kumfuata na kumwelezea azma yao aliona ni vyema kutoa kipaumbele ujenzi wa barabara ya eneo hilo, kwa kuwa inatumiwa na magari makubwa yanayotoka na kuingia bandarini.

Amesema kuwa imekuwa ni kampuni ya kwanza, kujitokeza kufanya ujenzi kwa gharama zao.

Ametoa mwito kwa wadau wengine, kujitokeza kuchangia miradi mbalimbali katika mkoa huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Atu Mwakitwange alisema kwa sasa wamemaliza hatua za mwanzo za ujenzi huo na ujenzi rasmi utaanza leo na itakamilika baada ya mwezi mmoja.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *