Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema serikali itatuma kikosi maalum cha kukabiliana na uvuvi haramu unaoendelea katika bahari ili kudhibiti na tatizo hilo ambalo limeathiri sana mazalia ya samaki na kuchangia kupungua kwa samaki baharini.

Makamu wa Rais amesema katika kuhakikisha kazi hiyo inafanyika vizuri serikali pia itatuma wataalamu wa mazingira ambao watafanya tathmini ya uharibifu wa mazingira katika bahari ili kujua uharibifu uliofanyika na kuchukua hatua ya kukabiliana na hali hiyo.

Ameeleza kuwa serikali itachukua hatua hizo ili kuinusuru bahari kwa sababu imekuwa ni chanzo kizuri cha mapato kwa wananchi kutokana na shughuli za uvuvi na shughuli nyingine zikiwemo za utalii.

Kuhusu uboreshaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Kilwa, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti zinazolenga kuhakikisha wananchi wote nchini wanapata huduma bora za afya katika ngazi zote.

Amesema mpango huo wa uboreshaji wa huduma za afya kwa wananchi nchini utaenda pamoja na utoaji wa elimu bora wa wanafunzi kote nchini chini ya mkakati wa serikali wa kutoa elimu bure kuanzia wanafunzi darasa la kwanza hadi kidato cha nne.Katika ziara yake mkoani Mtwara, Makamu wa Rais atazindua jengo la ofisi za Tume ya Maadili ya Uongozi wa Umma Kanda ya Kusini na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo.

Makamu wa Rais tayari amewasili mkoani Mtwara na kupokelewa na Viongozi mbalimbali wa mkoa huo wakiongozwa na Mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima Dendego pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angela Kairuki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *