Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amewataka wafugaji waache kutumika kama mtaji wa kisiasa kwani kufanya hivyo kutarudisha nyuma jitihada za kuimarisha na kuboresha shughuli zao nchini.
Samia Suluhu ametoa kauli hiyo Ikulu, Jijini Dar es Salaam baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa chama cha wafugaji nchini ambao walimpelekea kilio chao kuhusu matatizo na manyanyaso wanayoyapata wakiwa katika shughuli zao za ufugaji.
Makamu wa Rais, amesema amepokea mapendekezo ya wafugaji hao na serikali itafanyia kazi ili kuondoa hali ya sintofahamu na migogoro inayowakuta wafugaji katika maeneno mbalimbali nchini kwa sasa ikiwa ni pamoja na kuuunda kikosi kazi maalum ambacho kitafanya kazi ya kuchunguza matatizo mbalimbali li kuhakikisha suluhu ya matatizo hayo ikiwemo migogoro kati ya wafugani na wakulima inapatiwa ufumbuzi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Magembe Makoye ameiomba serikali kuwapatia mashamba makubwa ambayo hayajaendelezwa na wawekezaji ili nao waweze kufanya shughuli za ufugaji katika maeneo hayo.
Hata hivyo Magembe amesema kama serikali za mikoa na wilaya zote nchini zitaiga mfano wa mikoa ya Katavi na Ruvuma ambayo imeshatenga maeneo kwa ajili ya wakulima na wafugaji migogoro kama hivyo nchini itakuwa ni historia.