Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka Viongozi wa Mashirika ya Umma na Makampuni Binafsi kuwaruhusu wafanyakazi kushiriki michezo katika maeneo yao ya kazi lakini pia kuwaruhusu wafanyakazi hao kushiriki Michezo ya SHIMMUTA.
Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA) mjini Dodoma.
Makamu wa Rais amesema michezo ni muhimu sana kwenye Tanzania ya Viwanda kwani michezo husaidia mwili kuwa wenye afya bora na utendaji wao wa kazi unakuwa mzuri zaidi.
Makamu wa Rais amesema yeye alikuwa mwanamichezo mzuri wa mpira wa pete (Netball) lakini kwa sasa anafanya mazoezi kidogo kidogo asubuhi na jioni.
Makamu wa Rais aliwasihi Viongozi wa Michezo kusimamia masuala ya michezo katika maeneo ya kazi na kuwataka Viongozi wa Taasisi kuweka bajeti ya michezo kwa ajili ya kushiriki michezo ya SHIMMUTA.
Makamu wa Rais amesema ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya 2015- 2020 imeleekeza kuendeleza michezo sehemu za kazi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa SHIMMUTA, Ndugu Hamis Mkanachi alimpongeza Makamu wa Rais kwa juhudi anazozifanya katika kukuza michezo nchini.