Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi katika mradi mkubwa wa maji kwenye mji wa Nansio katika kisiwa cha Ukerewe mkoani Mwanza.
Mradi huo ambao unajumuisha kazi za uboreshaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira unatekelezwa chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Serikali ya Tanzania katika miji ya Sengerema, Geita na Nansio – Ukerewe kwa gharama ya Dola za Kimarekani milioni 30.4 ambapo serikali ya Tanzania imechangia mradi huo Dola za Kimarekani milioni nne.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amewaahidi wananchi kuwa serikali ya awamu ya tano ina mikakati mizuri inayolenga kuondoa tatizo la maji kote nchini ili kusaidia wananchi hao hasa wanawake kutumia muda mwingi kufanya kazi za maendeleo kuliko kutafuta maji.
Makamu wa rais amewahutubia wananchi wa kisiwa cha ukerewe kwenye kijiji cha Kagunguli mkoani Mwanza mara baada ya kuweka mawe ya msingi katika miradi miwili ukiwemo mradi wa maji na ujenzi wa chumba cha upasuaji katika kituo cha afya cha Kagunguli.