Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassani amezindua huduma mpya ya fedha mtandao ijulikanayo kama TTCL PESA ya Kampuni ya simu Tanzania TTCL.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na Omari Nundu ambaye ni Mwenyeketi wa Bodi ya TTCL, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Anjelina Madete, Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Waziri Kindamba na wajumbe wa Bodi  na wafanyakazi wa TTCL.

Makamu wa Rais amesema kuwa uzinduzi wa huduma ya TTCL PESA ni mwendelezo wa jitihada za Kampuni hiyo za kurejea katika nafasi yake ya awali ya kuwa suluhisho la kweli la utoaji huduma za Mawasiliano hapa nchini.

Pia amesema kuwa TTCL PESA itawezesha wananchi kutuma na kutoa pesa kwa viwango vya chini kupita mitandao yote, pia itawezesha wananchi kulipia Bill za Umeme (LUKU), Maji, Ving’amuzi na kuwezesha wateja kununua muda wa maongezi na vifurushi vya data vya TTCL.

Makamo wa Rais ameongeza kwa kusema kuwa TTCL PESA itatoa fursa kubwa ya ajira kwa wananchi kuwa mawakala na  itarahisisha shughuli za kiuchumi hasa biashara na hivyo aliwasihi wananchi kuonesha uzalendo wao kwa kutumia huduma za TTCL.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *