Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameelekea jijini Addis Ababa, Ethiopia kuhudhuria Mkutano wa 29 wa Wakuu wa  Nchi na Serikali  wa Umoja wa Afrika (AU).

Katika Mkutano huo wa siku mbili kuanzia tarehe 03-hadi 04 Julai-2017, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan atamuakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwenye mkutano huo.

Kabla ya ufunguzi rasmi, Mkutano huo ulitanguliwa na vikao vya Baraza la Utendaji linalowashirikisha Mawaziri wa Mambo ya Nje na Kamati ya Uwakilishi wa Kudumu  inayowahusisha Makatibu Wakuu wa Wizara za Mambo ya Nje kutoka nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika.

Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi  na Serikali  utafunguliwa rasmi leo tarehe 03-Julai-2017 katika Makao Makuu ya Umoja wa Afrika Jijini Addis Ababa, Ethiopia na  utajikita katika kujadili masuala mbalimbali yanayohusu umoja huo.

Miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika Mkutano huo ni pamoja na taarifa  kuhusu Maboresho katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na maboresho ya kitaasisi katika AU na  hali ya Ulinzi na Usalama katika bara la Afrika.

Kuhusu  hali ya  ulinzi na usalama katika Bara la Afrika majadiliano ya Viongozi hao yatajikita zaidi kwenye nchi za Sudan Kusini, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo- DRC na Libya.

Aidha, majadiliano hayo pia yatagusa  hali ya usalama kwenye baadhi ya nchi ambazo ziliathiriwa na kundi la Boko Haram za  Nigeria, Niger, Chad na Cameroon.

Mkutano huo 29 wa AU, unatarajiwa kuhuduhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *