Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Bill & Melinda Gates Foundation, Rodger Voorhies kwenye makazi ya Makamu wa Rais, Kilimani mjini Dodoma.

Makamu wa Rais amesema amezungumza mambo mengi na Bw. Rodger hasa kwenye masuala ya afya, uwezeshaji wanawake kiuchumi, kuwatoa kwenye kilimo cha sasa na kuwaingiza kwenye kilimo biashara lakini pia kuongeza thamani ya mazao na mambo ya masoko.

Makamu wa Rais alisema wamezungumza namna ya kuwarasimisha wanawake wa vijijini na wanawake wakulima ikiwa pamoja na uwezekano wa wanawake vijijini kuweza kupata mikopo.

Aidha Makamu wa Rais alizungumzia suala zima la upatikanaji wa maji safi na salama haswa kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam ambapo mara kwa mara kumekuwa na milipuko ya magojwa ya kipindu pindu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Bill & Melinda Gates Foundation Bw. Rodger Voorhies alisema wamekuja kwa Makamu wa Rais kuzungumza juu ya shughuli zinazofanywa na taasisi hiyo hapa nchini haswa katika masuala ya Kilimo na Afya na Mkakati Mpya wa Kuwawezesha Wanawake Kiuchumi.

Aidha wameipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua kubwa ambayo wamepiga katika kuwajumuisha wanawake katika masuala yanayohusu Fedha.

Mwisho, Mkurugenzi huyo ameahidi ushirikiano mkubwa kwa Serikali ya Tanzania katika kutekelezaji wa miradi ya taasisi yao.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *