Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameandika historia ya aina yake kwenda Dodoma kufanya ziara, ambapo ametumia njia ya barabara na kufanya mikutano kadhaa katika mikoa yote ya njiani ya Pwani na Morogoro.

Mtindo huo wa viongozi wa juu wa Serikali ya Awamu ya Tano, kusafiri kwa njia ya barabara, uliasisiwa na Rais John Magufuli ambaye mara kadhaa amesafiri kwenda Dodoma kwa njia ya barabara, safari ya umbali wa zaidi ya kilometa 470.

Juzi ilikuwa ni zamu ya Makamu wa Rais, ambapo njiani alifanya mikutano na wananchi katika miji ya Chalinze na Mlandizi mkoani Pwani, Msamvu mjini Morogoro na Gairo mkoani Morogoro.

Pamoja na kuzungumzia matatizo ya kimaeneo, safari ya barabara ya Makamu wa Rais jana ilibebwa na ujumbe mkubwa wa hatua zinazochukuliwa na serikali katika kukabili mapigano baina ya wakulima na wafugaji, yaliyoshamiri katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Dodoma na Manyara.

Akiwa Chalinze, Samia amesema ardhi isiwe chanzo cha umwagaji damu kutokana na mapigano ya wakulima na wafugaji. Bali, kila upande unapaswa kusimamia sheria na taratibu ili kuepusha hali hiyo; huku serikali ikiendelea na mipango ya kupima maeneo.

Amesema hivi sasa kumekuwa na migogoro ya wakulima na wafugaji, ambayo imesababisha vurugu, ambazo zinasababisha umwagaji wa damu, jambo ambalo serikali haitaki kuliona na kutaka kila upande kuheshimu sheria.

Amesema tataizo lingine ni baadhi ya wafugaji, kuwatumia watoto kuchunga mifugo na matokeo yake ni kushindwa kuidhibiti mifugo hiyo kuingia shambani na kufanya uharibifu wa mazao na kusababisha migogoro hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *