Vijana nchini wametakiwa kuhakikisha wanaitumia mitandao ya kijamii kutafuta maarifa yatakayowasaidia kuziishi itikadi na fikra za Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere zitakazosaidia kujenga Taifa imara na lenye nguvu.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira, January Makamba katika Kongamano la maadhimisho ya Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere katika Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kigamboni jijini Dar es salaam.
Makamba amesema Vijana wengi wamekuwa wakitumia mitandao ya Kijamii katika mambo yasiyo na tija kwao na kwa taifa na kuwataka kuyatafuta badala ya kutafuta maarifa ya waasisi wa Taifa kwa kusoma vitabu vyao pamoja na hotuba zao mbalimbali ambao yatawasidia kupata ufahamu na uelewa utakaojenga viongozi bora na madhubuti wa baadae
Amewataka vijana kote nchini kuiga mfano wa Mwalimu Nyerere wa moyo wa uzalendo katika kutetea uhuru wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni dhidi ya ukoloni mambo leo ambao umekuwa ukiteketeza rasilimali nyingi za taifa.
Baadhi ya watoa mada katika Kongamano hilo akiwemo mmoja wa wazee nchini Joseph Butiku amesema kuwa Mwalimu alisimamia mfumo wa vyama vingi nchini usiwe wa kujenga uhasama na chuki miongoni mwa wanasiasa bali kama nyenzo ya kuimarisha demokrasia ili kujenga Taifa lenye Umoja kwa misingi ya Heshima, Haki, Utawala bora na uwajibikaji.