Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuanzia Serikali itapiga marufuku utengenezaji wa pombe aina ya viroba ifikapo Machi mosi mwaka huu.
Ametoa kauli hiyo wakati akizumgumza na maelfu ya wakazi wa mji mdogo wa Mererani, wilayani Simanjiro akiwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Manyara.
Amesema agizo hilo linaenda sambamba na vita dhidi ya dawa za kulevya kwani mji wa Mererani unaongoza kwa matumizi ya dawa hizo haramu.
Kwa upande mwingine Waziri Mkuu amewaita wakurugenzi wa kampuni ya Tanzanite One ili wampatie taarifa juu ya malalamiko yanayotolewa na wafanyakazi wa kampuni hiyo kwamba hali ilikuwa nafuu wakati kampuni hiyo ikimilikiwa na wazungu kuliko hivi sasa.