Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Kassim Majaliwa amesema kuwa Rais, Dkt. John Magufuli hajawahi kutangaza ama kutoa kauli ya kufutwa kwa vyama vya siasa nchini.
Ametoa kauli hiyo leo Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Mbowe katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu.
Katika swali lake Mheshimiwa Mbowe alisema Rais Dkt. Magufuli alinukuliwa akisema atahakikisha anafuta vyama vyama vya upinzani na ifikapo mwaka 2020 hakuna upinzani nchini.
Pia Mheshimiwa Mbowe alitaka kujua nini kauli ya Serikali kuhusu kunyimwa dhamana kwa Mbunge wa Arusha Mjini, Mheshimiwa Godbless Lema ambaye anashikiliwa kwa muda miezi mitatu.
Mbali na Mheshimiwa Lema, pia kiongozi huyo alitaka kujua kuhusiana na kufungwa kwa Mbunge wa Kilombelo, Mheshimiwa Peter Lijualikali pamoja na madiwani sita wa chama hicho ambao wamefungwa na viongozi wengine 215 wanakabiliwa na kesi mbalimbali.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa “tunajua katika kuendesha nchi tunaendesha kwa mihimili mitatu ipo Serikali, Mahakama na Bunge na hakuna mhimili unaoweza kuuingilia mhimili mwingine,”.