Kiungo wa Algeria na klabu ya Leicester City, Riyad Mahrez amefanikiwa kushinda tuzo ya mchezaji bora wa Afrika wa BBC wa Mwaka 2016 baada ya kuwashinda wachezaji wenzake wanne.

Mashabiki kutoka kila pembe ya dunia walimpigia kura nyingi kiungo huyu wa kati wa Algeria na Leicester kuliko Pierre-Emerick Aubameyang, Andre Ayew, Sadio Mane na Yaya Toure.

Baada ya kupewa tuzo hiyo Mahrez amesema kuwa tuzo hiyo ina maana kubwa sana kwa sababu bila shaka yeye ni Mwafrika na ni jambo kuu sana kwa mchezaji wa Afrika kushinda tuzo hiyo.

Tuzo hii ni kilele kwenye mwaka mzuri kwa mchezaji huyu wa miaka 25, ambaye tayari amejishindia taji la Ligi ya Premia na alishinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka chaguo la Wachezaji Uingereza.

Mahrez ametambuliwa kwa uchezaji wake mzuri kama mchawi katika wingi, ambaye familia yake inatoka kijiji kidogo kwa jina El Khemis nchini Algeria, ambaye alitikisa Ligi ya Premia.

Mchezaji huyo ameisaidia Leicester City kushinda ligi bila kutarajiwa, ambapo alifunga mabao 17 na kusaidia ufungaji wa mabao 11 kuwawezesha kushinda, licha ya uwezekano wao kushinda mwanzoni mwa msimu kuwa 5000-1 pekee.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *