Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Balozi Dkt. Augustine Mahiga amesema Tanzania haina mpango wa kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).
Waziri huyo amesema kuwa Tanzania haina mpango wa kujiondoa katika Mahakama hiyo iliyoko The Hage nchini Uholanzi licha ya kwamba baadhi ya nchi barani Afrika zimeonesha nia ya kujitoa na kutokua na imani na utendaji kazi wa mahakama hiyo.
Amesema mpaka sasa hakuna sababu ya kujiondoa katika mahakama hiyo kwakuwa nchi haijafika mahali ambapo kuna watu au vikundi vya watu ambao wamehusika na makosa ya jinai, makosa ya kimbari, makosa dhidi ya binadamu au makosa ya kivita,hivyo Tanzania inaendelea kutafuta suluhu kwa kuona kama mahakama hiyo inaweza kufanyiwa marekebisho kwa baadhi ya sheria zake ili kuhimarisha utendaji wa haki na uwazi wa mahakama hiyo.
Amesema Tanzania haijaombwa kuunga mkono swala la kujitoa katika mahakama hiyo kwakuwa kulikuwa na mjadala wa nchi za Umoja wa Afrika zijiondoe kwa pamoja katika mahakama hiyo kwa umoja lakini hakukuwa na makubaliano wala muafaka wa jambo hilo hivyo hakuna sababu ya kujitoa katika mahakam hiyo.