Mahakama Kuu imesimamisha uamuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang’i wa kumtangaza mwanasheria machachari Miguna Miguna kuwa ni mhamiaji aliyepigwa marufuku.

Jaji Enoch Chacha Mwita Jumatatu kadhalika alisimamisha kufutwa kwa pasipoti ya Dk Miguna kulikofanywa na bosi wa uhamiaji Gordon Kihalangwa. Jaji huyo pia aliiamuru Idara ya Uhamiaji kusaidia kurudi kwa Dk Miguna kutoka Canada.

Aidha, Jaji ameliacha kama lilivyo tangazo la kwenye gazeti la serikali lililotolewa na Dk Matiang’i la kutangaza Vuguvugu la Taifa la Upinzani (NRM) ambalo ni tawi la muungano wa chama cha National Super Alliance (Nasa) kuwa kikundi cha uhalifu.

Jaji Mwita aliamua kwamba haki za Dk Miguna zilikiukwa kwa kufukuzwa kwake, na kwamba madai yaliyotolewa dhidi yake yanahitaji awepo yeye binafsi kujitetea.

Akisisitiza kuwa ushahidi kama huo hauwezi kutolewa kupitia hati ya kiapo, jaji aliamuru maofisa wa uhamiaji kumtumia Dk Miguna nyaraka za kumwezesha kusafiri.

Jaji aliamuru ikiwa zitakosekana nyaraka hizo kwamba anaweza kutumia pasipoti yake ya Canada, na kwamba anaweza kuja tarehe atakayoamua.

Jaji pia ameamuru pande husika katika kesi hiyo kuharakisha usikilizwaji akitaja kuwa ni kutokana na uharaka wa jambo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *