Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemfutia kesi ya kushambulia Naibu Waziri wa Fedha wa zamani, Adam Malima na dereva wake Ramadhan Mohammed.

Imeelezwa kwamba kesi hiyo imefutwa kwa sababu Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hana nia ya kuendelea na kesi hiyo, Malima ambae ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara amefutiwa kesi hiyo na Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage chini ya kifungu cha 91(1) cha Makosa ya Mwenendo wa Jinai.

Kabla ya kufutwa kwa kesi hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi alidai kuwa DPP hana nia ya kuendelea na kesi hiyo ambapo kutokana na hatua hiyo, Hakimu Mwijage alisema Mahakama hiyo imewaachia huru Washtakiwa hao.

Hakimu Mwijage amesema DPP kutokuwa na nia sio mwisho wa safari kwani amewaonea huruma tu, hivyo wawe makini ambao kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Malima anadaiwa kuwa May 15,2017 katika eneo la Masaki kwa makusudi alimzuia Ofisa wa Polisi mwenye namba  H.7818 PC Abdul kufanya kazi yake halali.

Malima anadaiwa kumzuia Ofisa huyo wa polisi kufanya kazi yake ya kumkamata Ramadhani Mohammed Kigwande kwa kosa la kumshambulia Mwita Joseph ambapo kwa upande wa Mshtakiwa wa kwanza, Kigwande, anakabiliwa na shtaka la kumshambulia Mwita Joseph.

Ilidaiwa kuwa siku hiyo ya Mei 15,2017 kwenye eneo hilo la Masaki wilaya ya Kinondoni mshtakiwa Ramadhani  akiwa na nia ya kumzuia Mwita Joseph ambaye ni Ofisa Oparesheni wa kampuni ya Priscane wakati alipokuwa akimkamata kwa kupaki vibaya gari namba T 587 DDL alimshambulia na kumsababishia maumivu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *