Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam imetoa kibali kwa Baraza la Wadhamini la Chama cha Wananchi (CUF) kufungua kesi dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, Profesa Ibrahimu Lipumba na wanachama wengine 12 waliosimamishwa uanachama.
Jaji Ama Isario Munisi alitoa kibali hicho jana baada ya kukubali hoja zilizotolewa na bodi hiyo kupitia kwa mawakili wao, Juma Nassoro na Hashimu Mziray.
Kwa mujibu wa sheria, bodi hiyo inapaswa kufungua kesi hiyo ndani ya siku 14, lakini tayari mawakili wanaoiwakilisha bodi hiyo, wamedai ndani ya siku saba watakuwa wamewasilisha kesi hiyo chini ya hati ya dharura ili isikilizwe haraka.
Maombi hayo namba 75 ya mwaka 2016, yaliwasilishwa mahakamani hapo Oktoba 5 mwaka huu, na jana yalisikilizwa na kutolewa uamuzi.
Bodi hiyo iliwasilisha maombi hayo ya kufungua kesi na kuiomba mahakama itoe amri ya kutaka Jaji Mutungi asijihusishe na masuala ya kisiasa nje ya Mamlaka, Kanuni na taratibu za Sheria ya Vyama vya Siasa.
Akitoa uamuzi, Jaji Munisi amesema amekubali maombi hayo na ameyapokea kwa mujibu wa sheria, pia mahakama imejiridhisha kuwa, maombi hayo yaliyokuwa na hati ya kiapo cha Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad baada ya kupitia nyaraka zilizowasilishwa.
Amesema amepokea maombi hayo baada ya kupitia nyaraka hizo za maombi na kuona zipo sahihi, hivyo waleta maombi wanapaswa kufungua kesi hiyo ndani ya siku 14 ikiwa na hoja muhimu wanazobishania.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa CUF Taifa, Twaha Taslima aliishukuru mahakama kwa kutoa kibali cha kufungua kesi na kuwataka wanachama watulie kwa kuwa suala hilo limefika kwenye mikono ya sheria.
Mwenyekiti wa Kamati ya Muda ya Uongozi wa CUF, Julius Mtatiro alisema wamesikitishwa na barua ya Jaji Mutungi kwenda kwenye benki mbalimbali ikiwamo ya NMB tawi la Ilala, kufungua akaunti nyingine ya chama huku akifahamu kikatiba hairuhusiwi.