Mahakama Kuu imeamuru aliyekuwa Naibu waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana katika Serikali ya awamu ya nne, Dkt. Makongoro Mahanga kukamatwa na kufikishwa mahakamani hapo.
Amri hiyo imetolewa na Naibu Msajiri wa Wilaya, Mahakama Kuu Ruth Masambu wiki iliyopita baada ya Mahanga kushindwa kufika mahakamani hapo bila taarifa.
Dkt. Mahanga alitakiwa kufika mahakamani hapo siku ya Alhamis ili kulipa deni la shilingi milioni 2 ikiwa ni sehemu ya deni la milioni 11 anazodaiwa.
Mahanga anadaiwa na mwanaharakati wa haki za binadamu nchini Kainerugaba Msemakweli ikiwa gharama ya alizotumia katika kesi ya madai ya kashfa iliyofunguliwa dhidi yake na Dkt. Mahanga.
Mahanga alifungua kesi ya madai mwaka 2009 akidai kuwa kitabu alichoandika mwanaharakati cha ‘Orodha ya Mafisadi wa Elimu Tanzania’ kikimtaja kuwa mmoja wa vigogo wenye shahada ya Udaktari wa Falsafa wa kughushi, kilimdhalilissha.